AfD yajitenga na matamshi ya chuki ya msemaji wake
29 Septemba 2020Mapema, gazeti la Zeit lilikuwa limeripoti kwamba Lüth alizungumzia juu ya "kuwapiga risasi na kuwachoma kwa gesi ya sumu" wahamiaji mnamo mwezi Februari, wakati huo akiwa msemaji wa AfD, alipokutana na mmoja wa wanawake mashuhuri kwenye mitandao ya kijamii, Lisa Licentia, katika baa moja mjini Berlin na matamshi hayo kurushwa kwenye filamu fupi iliyooneshwa na kituo kikubwa cha televisheni nchini Ujerumani, ProSieben, jioni ya Jumatatu (Septemba 28).
Lakini jioni hiyo hiyo, mwenyekiti mwenza wa kundi la wabunge wa chama hicho, Alexander Gauland, alikitenga mbali chama hicho cha mrengo mkali wa kulia na matamshi hayo, akisema "hayakubaliki na hayaendani na dhamira na sera za AfD."
Kwenye taarifa yake kwa umma, Gauland, ambaye chama chake kinatumia jukwaa la chuki kwa wageni kuzidi kujizolea umashuhuri katika kila uchaguzi unaofanyika, alisema "hata kuyataja tu matamshi hayo ni matusi na upotofu mkubwa," kwa chama hicho.
AfD iliingia bungeni mwaka 2017 na sasa kinaongoza kambi ya upinzani dhidi ya muungano mkuu unaovijumuisha vyama vikubwa vya kihafidhina na mrengo wa kushoto - CDU, CSU na SPD.
Nini hasa kimo kwenye matamshi hayo
Wakati alipokutana na Lisa Licentia katika baa ya Newton mjini Berlin tarehe 23 Februari, Lüth anaripotiwa kumwambia kwamba AfD ilitumia mbinu za uchokozi.
"Kila mambo yakiwa mabaya kwa Ujerumani, ndivyo yanavyokuwa mazuri kwa AfD", alinukuliwa akisema, huku akiongeza kwamba kama isingelikuwa hivyo, chama hicho kingelikuwa kinapata asimilia tatu tu kwenye chaguzi.
Alipoulizwa na Lisa ikiwa ni jambo lenye maslahi kwa AfD endapo wahamiaji wengi zaidi wanakuja Ujerumani, Lüth alijibu kwamba ni sawa, kwani AfD huwa inafanya vyema zaidi katika hali hiyo.
"Baadaye tunaweza kuwapiga risasi wote. Hilo si tatizo hata kidogo. Au kuwaunguza kwa gesi ya sumu, au lolote utakalo. Kwangu mimi sawa sawa tu." Alinukuliwa akisema.
Kufukuzwa kazi
Kwa mujibu wa vyombo vya habari hapa Ujerumani, Lüth ameondoshwa kwenye nafasi yake kama mwajiriwa wa kundi la wabunge wa chama hicho bungeni.
Awali, alikuwa amesitishwa nafasi yake kama msemaji wa chama mwezi Aprili, baada ya barua pepe aliyoandika kwamba neno "fashisti" limekuwa likitiwa chumvi.
Ingawa kituo cha televisheni cha ProSieben hakikumtambulisha afisa huyo wa juu wa AfD, lakini ilirikodi filamu hiyo fupi kwa jina "Mrengo Mkali wa Kulia, Mjerumani, Mwenye Siasa Kali."
Kwa upande wake, gazeti la Zeit lilisema liliamuwa kuliweka hadharani jina hilo baada ya utafiti wake wa kina kwa sababu ya maslahi ya umma.
Filamu hiyo fupi ilitokana na utafiti wa miezi 18 kwenye makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia uliofanywa na mwandishi wa habari Thilo Mischke, akiuliza endapo demokrasia ya kiliberali nchini Ujerumani ipo hatarini!