1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adhabu ya Kifo yaongezeka Duniani

P.Martin18 Mei 2007

Wanaharakati nchini Iran wamepania kuufahamisha umma kuwa adhabu ya kifo haisaidii kuzuia uhalifu na yapaswa kuondoshwa,kwa sababu ni katili.

https://p.dw.com/p/CHku

Wanaharakati hao wameamua kufanya kampeni dhidi ya adhabu ya kifo nchini Iran,baada ya wafungwa 177 waliopewa adhabu ya kifo,kuuliwa katika mwaka 2006.Takwimu hiyo imechapishwa katika ripoti mpya inayohusika na adhabu ya kifo kote duniani na kutolewa na shirika linalotetea haki za binadamu duniani-Amnesty International.Kuambatana na takwimu rasmi,China imeshika nafasi ya kwanza, baada ya adhabu hiyo kutekelezwa mara 1,010 nchini humo.Lakini wanaharakati wanasema,idadi halisi huenda ikawa mara nane zaidi.Takwimu zinazohusika na Iran,zimekusanywa kutokana na ripoti za vyombo vya habari na wanaharakati,kwani serikali haitangazi,idadi ya vifo vya aina hiyo.

Kwa upande mwingine,ripoti ya “Amnesty International” inaonyesha kuwa kote duniani kwa jumla,idadi ya wafungwa waliouliwa imepunguka ikilinganishwa na mwaka 2005.Lakini nchini Iran, hali ya mambo ni kinyume.Hata mwaka huu,hakuna ishara kuwa idadi hiyo inapunguka.Kwa mfano, wagombea haki za binadamu wanasema,vyombo vya habari vimeripoti kwamba watu 18 wameuliwa katika kipindi cha majuma mawili,mwezi huu wa Mei.

Mgombea haki za binadamu aliekataza kutajwa kwa jina amesema,kuondosha sheria zote zinazohusika na adhabu ya kifo nchini Iran kwa hivi sasa ni kama ndoto.Sababu ni kwamba nchini humo,adhabu ya kifo huchukuliwa kuwa ni muhimu ili kuzuia uhalifu katika jamii.

Kwa hivyo,ujumbe mkuu wa wanaharakati nchini Iran hivi sasa,ni kuifahamisha jamii kwamba kutekelezwa kwa idadi kubwa ya adhabu ya kifo hakumaanishi kuwa uhalifu hupunguka.Kwa maoni ya wagombea haki za binadamu,ni muhimu pia kuwa na kampeni ya kuishinikiza serikali,kupunguza idadi ya adhabu hiyo.

Nchini Iran hivi sasa,makosa yanayoadhibiwa kifo yanahusika na mauaji,madawa ya kulevya, itikadi,uhalifu wa kifedha na hata ya kijinsia.Kawaida adhabu hiyo ya kifo hutekelezwa kwa kunyongwa na mara nyingine hata hufanywa hadharani.

Msingi wa mfumo wa kisheria nchini Iran,unahusika na sheria za Kiislamu.Sheria zote zinazopitishwa na bunge zinahitaji pia kuidhinishwa na baraza la viongozi sita wa kidini wenye itikadi kali,likiwa na usemi mkubwa.Likiongozwa na mkuu wa dini Ayatollah Khamenei,baraza hilo huchunguza ikiwa sheria zote zinaambatana na sheria za kidini. Baraza hilo,kwa kutumia kura ya turufu,linaweza kuzuia sheria zinazopitishwa na bunge.

Hivi sasa nchini Iran,mwanaharakati Emadeddin Baghi anafanya kampeni ya kuwashawishi wabunge na viongozi wa kidini kuondosha adhabu ya kifo au itumiwe kwa nadra tu.Baghi alie mfuasi wa dhati wa dini ya Kiislamu aliwahi kuwa mwanafunzi katika shule ya dini ya Qom.Mwanaharakati huyo anasema uhalali wa imani yake kuhusu “haki ya kuishi” pamoja na kuondoshwa adhabu ya kifo, unakutikana katika Koran na sheria za Kiislamu. Mgombea huyo wa haki za binadamu,sasa ameandika kitabu juu ya adhabu ya kifo na dini ya Kiislamu. Hoja yake kuu ni kuwa,kuondoshwa adhabu ya kifo si kinyume na dini ya Kiislamu.