ACT Wazalendo chataka miji mikubwa kufungwa Tanzania
15 Aprili 2020Chama hicho cha kisiasa kimetoa mapendekezo ya wazi kwa serikali juu ya hatua za kuchukua ili kupunguza madhara ya virusi vya Corona katika kipindi hiki ambacho bado dunia inatafuta mbinu za kuutokomeza ugonjwa ugonjwa huo uliogharimu maisha ya watu zaidi ya laki moja na elfu ishirini ulimwenguni.
Taarifa rasmi ya serikali inaonesha vifo vya watu wanne kutokana na ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa virusi hivyo vya corona, ambapo watatu ni kutoka Tanzania bara na mmoja kutoka Zanzibar.
Chama cha ACT wazalendo kimependekeza serikali ifunge mikoa yenye shughuli nyingi za kiuchumi na yenye idadi kubwa ya watu ukiwemo mji mkuu wa kibiashara Dar es salaam, Mwanza, Arusha na mji wa kiutalawa Dodoma, huku wakitoa ushauri namna ambavyo serikali itawasaidia wananchi kuhimili hatua hizi za vizuizi kwa muda wa miezi mitatu katika maeneo hayo.
Visa vya maambukiizi ya virusi vya Corona vimepundikia hamsini nchini Tanzania
Chama hicho pia kimependekeza kuachiwa kwa wafungwa magerezani hasa wale ambae wana umri wa zaidi ya miaka 65, waliohukumiwa kwa makosa ya kudhaminika, wanawake wajawazito pamoja na wale wenye watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, hatua waliioitaja ni katika kupunguza mrundikano wa wafungwa katika magereza.
Kwa upande wa Zanzibar chama hicho kimeyataja makampuni ya utalii kuwa wahanga wakubwa wa mlipuko wa virusi vya corona na kupendekeza serikali kupitia mashirika ya hifadhi ya jamii, yawalipe wafanyakazi wa makampuni hayo ambayo kwa hivi sasa hayana uwezo wa kuwalipa wafanyakazi kutokana na watalii wengi kufuta safari zao.
Tanzania hivi karibuni imetangaza hatua zaidi za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona kwa kuzuia safari zote za ndege za abiria kuingia na kutoka nchini pia kuendelea kuzifunga taasisi za elimu kwa kipindi kisicho julikana miongoni mwa nyingine.
Mandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam