Abiy awataka raia kupambana na vikosi vya Tigray
11 Agosti 2021Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametoa kauli siku ya Jumanne kuwahimiza raia wa nchi hiyo kujiunga na jeshi kuwachakaza wapiganaji wa vikosi vya Tigray wanaoendeleza mapambano. Wito huo umewashitua Watigray hata wale wanaoishi nje ya nchi, huku Abiy akiwataka Waethiopia wawe macho na masikio ya nchi ili kuwafuatilia na kuwafichua majasusi na mawakala wa vikosi vya Tigray. Watu walioshuhudia na mawakili wamesema maalfu wa Watigray tayari wamekamatwa na wanazuiliwa wakati wa mzozo kutokana na utambulisho wao pekee.
Teklehaymanot G. Weldenmichel, ambaye familia yake imenasa Tigray, anasema aina ya vita anavyoitisha waziri mkuu viko katika ngazi nyingine tofauti kabisa wito wake ukiwa na maana ya kusafisha kila mtu.
Wito wa kujiunga na vita kwa sasa si wa lazima lakini kwa sababu watu wamezuiwa kuyafikia maeneo mengi ya Ethiopia, ni vigumu kufahamu aina ya shinikizo linalotumika. Kauli ya Abiy imetolewa wakati shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR likisema limefanikiwa kuzifikia kambi za wakimbizi katika eneo la Tigray.
Hali bado ni ngumu Tigray
Akizungumza mjini Geneva, msemaji wa UNHCR, Boris Cheshirkov amesema, "UNHCR na washirika wake wamefanikiwa kuingia kambi za wakimbizi wa Eritrea za Mai Aini na Adi Harush katika eneo la Tigray. Hata hivyo hali ya usalama bado inakwamisha kuyafikia maeneo mengi na wakimbizi wanaendelea kukabiliwa na hali ngumu. Huduma za msingi kama vile matibabu na huduma za afya bado hazipatikani na maji safi ya kunywa yanakaribia kuisha."
Wito wa utanuzi wa vita Ethiopia umewatia wasiwasi baadhi ya watu wa makabila mengine kama vile Amhara, ambao wanahofia vikosi vya Tigray, ambavyo sasa viko kwenye mapambano, vitafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi. Demissie Alemayehu, profesa anayeishi Marekani aliyezaliwa katika eneo la Amhara alisema muda mfupi baada ya wito wa waziri mkuu Abiy Ahmed kwamba vikosi vya Tigray vimejihami vyema na silaha na watakaopata hasara kubwa kwa mara nyingine ni watu wa Amhara. Profesa huyo ameongeza kusema bila kuyashughulikia matatizo ya msingi yanayoikabili Ethiopia, likiwemo suala la katiba iliyojikita kwa misingi ya tofauti za kikabila, itakuwa vigumu mno kuzungumzia amani.
Naibu Mkuu wa serikali ya eneo la Amhara, Fenta Mandefro, amesisitiza kuwa mamia ya wakazi wa Amhara tayari wameshauwawa na wengine wengi watakabiliwa na hatari ya kuangamia iwapo wataendelea kuuheshimu na kuutekeleza mkataba wa usitishaji mapigano ambao umeshatupwa kapuni na vikosi vya Tigray.
(ap, afpe)