1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy Ahmed akanusha watu kufa kwa njaa Ethiopia

7 Februari 2024

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amekanusha kuwa watu wanakufa njaa katika taifa hilo la Pembe ya Afrika ambalo linakabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula unaosababishwa na mizozo ya ndani na majanga ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/4c7cU
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.Picha: United Nations FAO 2024

Ahmed ametoa maelezo hayo kwa wabunge baada ya kutolewa tahadhari kwamba idadi ya watu ambao wanakabiliwa na uhaba wa chakula inaweza kufikia milioni 11 baadaye mwaka huu katika nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Hata hivyo, kiongozi huyo amekiri kwamba inawezekana watu wamekufa kutokana na magonjwa yanayohusishwa na utapiamlo.

Soma zaidi: Je, mzozo wa njaa unaweza kuepukika nchini Ethiopia?

Uongozi katika jimbo la Tigray ulionya mwezi Desemba juu ya hatari ya kuzuka baa la njaa kutokana na ukame na athari za vita vinavyoendelea kwa miaka miwili katika eneo hilo.

Awali, taarifa ya pamoja ya Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Kudhibiti Majanga nchini Ethiopia, Shiferaw Teklemariam, na Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu nchini humo, Ramiz Alakbarov, imesema maisha ya mamilioni ya watu na mifugo yameathirika kutokana na uhaba wa chakula unaotisha na kuongezeka kwa utapiamlo.