1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2015 yavunja rekodi kwa adhabu za vifo zilizotekelezwa

6 Aprili 2016

Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International inaonyesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka uliopita katika utekelezaji wa hukumu ya kifo, ilikuwa kubwa zaidi tangu mwaka 1990.

https://p.dw.com/p/1IQ6l
Kumekuwepo ongezeko la asilimia 50 katika utekelezaji wa adhabu ya kifo mwaka 2015
Kumekuwepo ongezeko la asilimia 50 katika utekelezaji wa adhabu ya kifo mwaka 2015Picha: AP

Kulingana na ripoti hiyo ya shirika la Amnesty International iliyochapishwa Jumatano, idadi ya waliouwa mwaka 2015 katika kutekeleza adhabu ya kifo waliyohukumiwa ilikuwa watu 1,634, bila kujumuisha wale waliouawa nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo hubakia kuwa siri.

Mtaalamu wa masuala yanayohusiana na adhabu ya kifo, Oliver Hendrich wa tawi la Amnesty International nchini Ujerumani, amesema idadi hiyo kubwa inaonyesha ongezeko la asilimia zaidi ya 50 ikilinganishwa na watu waliouawa mwaka 2014.

Mkurugenzi wa Amnesty International anayehusika na masuala ya kimataifa Audrey Gaughran, amesema kwamba asilimia kubwa ya adhabu hizo za vifo zilizotekelezwa, inatoka katika nchi tatu tu.

''Ongezeko la kutisha la kutekelezwa kwa adhabu ya kifo lililoshuhudiwa mwaka jana, lilisababishwa na idadi kubwa sana ya waliouawa nchini Iran, Pakistan na Saudi Arabia. Asilimia zaidi ya 90 ya adhabu za vifo zilizotekelezwa, ukiondoa nchini China, ilikuwa katika nchi hizo tatu''. Amesema Gaughran.

Sababu tofauti kati ya nchi na nchi

Nchini Iran pekee, watu 977 waliuawa katika kutekeleza hukumu yao ya kifo, wengi wao kutokana na hatia zinazohusiana na madawa ya kulevya, imeonyesha ripoti ya Amnesty International. Hali kadhalika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 320 waliuawa nchini Pakistan, huku Saudi Arabia ikitekeleza adhabu ya kifo dhidi ya watu 158 mnamo mwaka 2015.

Maandamano ya kupinga adhabu ya kifo nchini Iran
Maandamano ya kupinga adhabu ya kifo nchini IranPicha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Nchini Saudi Arabia, takribani nusu ya watu wanaouawa tangu miaka ya 1980 wanakuwa ni wageni, hususan wale wanaoingia nchini humo kutafuta ajira, ambao aghalabu ufahamu wao wa lugha ya kiarabu ni haba, na hawana usaidizi kisheria.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba adhabu za vifo zilizotekelezwa nchini Marekani zilikuwa 28, hiyo ikiwa idadi ndogo zaidi tangu mwaka 1991.

China ambayo hukadiriwa kutekeleza maelfu ya adhabu za vifo kila mwaka huwa haichapishi takwimu zake, mkurugenzi wa Amnesty International katika ukanda wa Asia Mashariki Nicholas Baquelin anasema China inafahamu fika kuwa ikiwa idadi ya watu inaowauwa kila mwaka itawekwa wazi, hadhi yake itaingia doa machoni mwa walimwengu.

Kwa mara ya kwanza nchi zisizo na adhabu ya kifo zimekuwa nyingi kuliko zinaikumbatia adhabu hiyo.
Kwa mara ya kwanza nchi zisizo na adhabu ya kifo zimekuwa nyingi kuliko zinaikumbatia adhabu hiyo.

Matumaini yapo licha ya misiba

Pengine habari njema kwa mwaka uliopita, kulingana na ripoti hiyo ya Amnesty international, ni kwamba mwaka huo wa 2015 ulishuhudia pia idadi kubwa ya nchi zilizoiondoa hukumu ya kifo katika sheria zake. Madagascar, Jamhuri ya Kongo, Fiji na Suriname ziliifuta kabisa hukumu, na kuifanya idadi ya nchi ambazo hazina tena hukumu ya kifo kufikia 102 duniani kote.

Kwa idadi hiyo, kwa mara ya kwanza nchi zisizo na huku ya kifo ni nyingi kuliko zile zinazoendelea kuikumbatia.

Hata nchini China, shirika la Amnesty International limesema zipo dalili kuwa idadi ya watu ambao hukumu yao ya kifo ilitekelezwa ilipungua mwaka jana ikilinganishwa na miaka iliyopita, ingawa shirika hilo halikuweza kuthibitisha hali hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre/ape

Mhariri:Iddi Ssessanga