140 wauwawa katika mashambulizi ya Syria
22 Februari 2016Umwagaji damu umezidi kuongezeka nchini Syria wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akisema makubaliano ya muda yamefikiwa yenye kuzingatia hatua za suluhu kwa mzozo huo wa miaka mitano nchini Syria wenye kusababisha maafa makubwa.
Karibu na mji mkuu Damscus mripuko wa gari ukifuatiwa na mashambulizi mawili ya kujitowa muhanga karibu na kaburi takatifu la Washia la Seyyida Zeinab ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad yameuwa watu 83 hapo jana.
Shirika la habari la serikali SANA limeripoti kwamba watu 178 wakiwemo watoto wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ambayo yametokea wakati wanafunzi walipokuwa wakitoka shule katika eneo hilo.
Kuendelea kwa maafa
Takriban maduka sitini yameharibiwa na magari magari kuteketezwa kabisa.Hapo mwezi wa Januari shambulio linalodaiwa pia kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu katika eneo hilo hilo limeuwa watu sabini.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London Uingereza pia limeripoti kwamba miripuko miwili ya mabomu yaliotegwa kwenye magari imeuwa watu 59 na kujeruhi wengine kadhaa katika kitongoji chenye wafuasi wengi wa serikali cha Al Zahraa katika mji wa kati wa Holms.
Al-Zahraa ambapo wengi wa wakaazi wake wanatokea kabila la madhebu ya Kishia la Alawi anakotokea Rais wa nchi hiyo Bashar al Assad imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara.
Shinikizo la mataifa makubwa
Mataifa yenye nguvu duniani yamekuwa yakishinkiza usitishaji wa uhasama wa takriban miaka mitano ya vita vya Syria na yalitaraji kuanza kwa suluhu hiyo hapo Ijumaa lakini iliwawia vigumu kukubaliana juu ya masharti ya kusitisha uhasama huo.
Hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Segei Lavrov sio chini ya mara tatu kujaribu kukubaliana juu ya masharti hayo.
Kerry amesema ""Nilisisitiza juu ya haja ya dharura kufanikisha usitishaji kamili wa uhasama katika kipindi cha muda mfupi kadri inavyowezekana.Na ninaamini kwamba kupitia mazungumzo haya tumefikia makubaliano ya muda".
Kerry alitowa kauli hiyo hapo jana wakati akiwa Amman nchini Jordan.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi baadae ilisema Lavrov na Kerry walikuwa na mazungumzo ya simu zaidi ya mara mbili na kukamilisha masharti ya kusitisha mapigano ambayo yatawasilishwa kwa marais wao.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri :Yusuf Saumu