1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Polisi DRC yakamata washukiwa wa mauaji ya balozi wa Italia

19 Januari 2022

Polisi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametangaza kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na shambulizi ambamo balozi wa Italia Luca Attanasio aliuawa mnamo Februari 22 mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/45l6Y
DR Kongo | Luca Attanasio, ermordeter italienischer Botschafter
Picha: FOTOGRAMMA/IPA/picture alliance

Jenerali Aba Van Ang, Kamishna wa polisi katika mkoa wa Kivu Kaskazini, alisema waasi walimuua Balozi Luca Attanasio katika jaribio lililotibuka la kumteka kwa ajili ya kikomboleo.

"Bwana Gavana, ninawasilisha kwako makundi matatu ya wahalifu ambayo yalisababisha maafa katika mji wa Goma. Miongoni mwao, kundi lililoushambulia msafara wa balozi wa Italia na kumuua," alisema Jenerali Ang wakati wa tukio lililohudhuriwa na baadhi ya waandishi habari mjini Goma.

Washukiwa hao ambao waliwasilishwa kwa gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini siku ya Jumanne, walikuwa wapenga kuomba kikomboleo cha dola milioni moja, walisema maafisa.

DRK Nach Überfall auf Konvoi von Luca Attanasio
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO, kikichukua miili kutoka vichakani, baada ya msafara wa balozi Attanasio kuvamiwa na balozi huyo pamoja na mlinzi wake na dereva wa WFP kuuawa, Februari 22, 2021.Picha: Justin Kabumba/AP/dpa/picture alliance

Badala yake, balozi huyo aliekuwa na umri wa miaka 43, alipigwa risasi iliyokatisha uhai wake pamoja na afisa wa kijeshi Vittorio lacovacci, na dereva wa shirika la kimataifa la chakula Moustapha Milambo.

Soma pia: Mauaji ya balozi wa Italia yazusha mzozo wa Italia na DRC

Haikubainika mara moja lini ukamataji huo ulifanyika au lini mashtaka yataanza. Mshukiwa mkuu katika mauaji ya balozi huyo, alietambulika kwa jina la Aspirant, anaendelea kujificha, imsema polisi.

Jenerali Van Ang alisema kundi la watu hao waliokamatwa katika mazingira ambayo hayakutajwa, pia walihusika na vitendo vya utekaji nyara wa hivi karibuni katika eneo hilo, haswa  vilivyowalenga wanachama wa mashirika ya kibinadamu.

"Makundi" mengine mawili yaliyowasilishwa kwa gavana huyo yanashutumiwa na polisi kwa kufanya mauaji mbalimbali na mashambulizi ya kinyama. Ametoa wito kwamba wahalifu hao waadhibiwe kulingana na yote ambayo wamesababisha kwa wananchi.

Siku ya Jumanne, polisi pia iliwasilisha wanaume wengine wanne wanaotuhumiwa kwa kuwashambulia wafanyakazi wengine wa misaada katika eneo hilo.

DR Kongo Militärischer Gouverneur von Nord-Kivu Constant Ndima
GAvana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Congo Mashariki, Constant Ndima. Picha: Benjamin Kasembe/DW

Soma pia:Italia yataka uchunguzi mauaji ya balozi wake DRC 

Italia iliuomba rasmi Umoja wa Mataifa, UN, kuanzisha uchunguzi juu ya kilichotokea, katikati mwa maswali kuhusu iwapo mipango ya ulinzi ya UN ilikuwa ya kutosha kwa ajili ya ujumbe huo.

Umoja wa Mataifa umesema barabra ilikuwa imeidhinishwa kwa ajili ya safari bila wasindikizaji wa kiusalama au magari ya kijeshi.

Mwezi Juni mwaka uliopita, Italia ilianzisha uchunguzi dhidi ya afisa wa Kongo wa shirika la WFP ambaye, kulingana na vyombo vya habari vya nchi hiyo, alikuwa anahusika na hatua za kiusalama wakati wa msafara huo.

Msafara huo ulikuwa unatoka Goma kwenda Rutshuru, ambako balozi alipaswa kutembelea mradi wa WFP unaowapatia chakula wanafunzi kwenye shule.